1/17/23

Mbinu mojawapo ya kumaliza upungu wa umeme nchini


Mnamo tarehe 1 na 2 Novemba 2022 kulikuwa na kongamano la Nishati Safi ya kupikia, lililofanyika mkoani Dar es Salaam, kama lilivyorusha kwenye vyombo mbalimbali vya habari Tanzania na nje ya Tanzania. Kwenye hilo kongamano wadau waliongelea kupika kwa kutumia umeme. Walisema ni njia rahisi na ya haraka kwa kuwa kwa sasa kuna vifaa vya kisasa vya kupikia kwa umeme na vina ufanisi mkubwa. Wengi walikuwa na wasiwasi na huu mgao unaoendelea sasa nchini, kwamba unaweza kuweka chakula chako jikoni halafu umeme ukakatika na ukashinda njaa. Wachangia mada wengine walisema kupika kwa umeme sio kwamba tu ni ghali, ila umeme hautoshelezi (ni wa mgao).
Kuhusu upungufu wa umeme, nina ushauri ufuatao ambao unatufaa sana kwa muda mfupi ujao. Mbinu mojawapo ambayo inaweza kutusaidia kuzalisha umeme ni kuzalisha umeme na joto kwa wakati mmoja (Combined Heat and Power) kwa kutumia takataka tunazozalisha mitaani. Kila wilaya na kila mkoa una dampo/jaa la takataka. Kwenye haya madampo inawezekana kuweka mitambo ya kuchoma taka (baada ya kuzichambua na kuzitenganisha) na kuzalisha mvuke ambao unaendesha mifuo ya umeme. Teknolojia hii si ngeni na kwa hapa Tanzania inatumika Mkoani Njombe (Tanwat) na TPC mkoani Kilimanjaro. Tanwat wanatumia masalia ya miti baada ya kuvunamiti ya nguzo, badala ya taka, TPC wanatumia masalia ya miwa badala ya taka za mtaani. Iwapo mitambo hii tungeiweka kila mkoa (inawezekana iwapo tutaipa kipaumbele), tusingekuwa na upungufu wa umeme tunaolalamikia kila leo. Kutegemea umeme wa maji kwa enzi hizi si wazo endelevu hata kidogo, kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha kukauka kwa mito mingi na hivyo kuathiri sana uzalishaji wa umeme. Wazo jingine lenye uwezekano ni kutumia umeme wa jua na upepo. Kampuni ya Rift Valley Energy tayari wamefunga mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo wilayani Mufindi mkoani Iringa. Inawezekana pia kuzalisha umeme mahali pengine penye upepo.
 
Pichani (nyuma yangu) ni mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia takataka zilizochambuliwa. Unamilikiwa na Manispaa ya Mji wa Karlstad, Sweden.
 


 

6/13/18

MAWE YA ILULA YAZUA MJADALA

Hii ni picha ya eneo la Ilula, mkoani Iringa. Uharibifu wa mazingira umesababisha kilele cha mlima huo kukosa miti. Picha ya Maggid Mjengwa.


UTANGULIZIKaribu katika mjadala ndugu mwanablogu mwenzangu. Niweke wazi kwamba mjadala huu ni mwendelezo wa mada iliyoanzishwa katika blogu ya mwanakijiji Maggid Mjengwa kuhusu mawe yaliyopo katika eneo la Ilula. Mada yenyewe katika blogu hio inasema hivi, nanukuu Kuna mwanakijiji mwenzetu aliyefikiri, kuwa Iringa "IMEBARIKIWA" kwa mawe. Lakini, mlima huo na mingine ya hapa Iringa ilifunikwa na misitu kabla. Kinachoonekana hapo n i uharibifu wa mazingira. Miti yote imekatwa. Kuna vijana wa Iringa wanaokumbuka, kuwa hadi mwaka 1977, waliweza kupanda milima hiyo iliyokuwa na miti mingi. Walikwenda huko na kuwinda ngedere wakiwa na mbwa wao. Binafsi nakumbuka utotoni. Miaka ile ya mwanzoni mwa 70's nikiwa na baba yangu tulisafiri kwa basi la KAMATA toka Igawa Mbeya hadi Iringa. Hapo tulikaa siku kadhaa kwa ndugu yetu mmoja aliyeitwa Merere. Ndugu huyu aliishi Gangilonga, ilijulikana pia kama "Uzunguni". Naikumbuka Iringa iliyokuwa na miti mingi. Mawe hayo ya mlimani sikumbuki kama niliyaona. Nakumbuka Gangilonga yenyewe ilikuwa imefunikwa na miti mingi.Nilipofika tena Iringa miaka ya 90 nikamwuliza mwenyeji wangu nikikumbuka Gangilonga ya utotoni; " Hivi Gangilonga ni wapi ? Niliuliza. " Hapa ulipo ndio Gangilonga!" Alinijibu. Naam. Tunakaribisha mawazo kutoka kwenu, juu ya namna gani tunaweza "kuikijanisha" tena Iringa na hatimaye kuyafunika tena mawe hayo yanayoonekana. Mwisho wa kunukuu.
Kiungo cha mada hio ni http://mjengwa.blogspot.com/2007/08/baraka-au-laana.html
Mtazamo ninaouandika hapa ni wangu, hivyo niko tayari kusahihishwa, kushauriwa ama kukosolewa. Karibuni!

Wanakijiji wanataka huo mlima wa Ilula ufinikwe na mimea kama inavyonyesha picha hii. Inawezekana, tutimize wajibu wetu!
MJADALAUtangulizi huo hapo juu ndio uliozua gumzo na majadala mkali miongoni mwa wachangiaji. Wengi wa wachangiaji walianza na hitimisho kwanza, kuwa ni lazima mimea ipandwe mahali pale ili pawe na ukijani kama ilivyokuwa hapo mwanzo, kama ilivyoshuhudiwa na mmoja wa wanakijiji aliyepita mahali hapo miaka hiyo ya ’70. Shida ilikuwa ni namna gani ya kuanza ’kupakijanisha’ mahali hapo. Na ukiangalia picha hio kwa umakini utaona kuwa kando ya hizo nyumba chini ya huo mlima kuna miti na inaonyesha kuwa ina afya njema tu. Sina uhakika kuwa miti hiyo ni ya kupandwa ama ya asili (nitatembelea hapo mahali na kutoa jibu), lakini kuna dalili zote kuwa hapo mahali miti inasitawi.

HOJA
1. PENDEKEZO LA KUGAWA MITI KWA WANANCHI

Baadhi ya wanakijiji walishauri kugawa miche ya miti kwa wakazi wa Iringa mjini, vyuoni na kwa wanafunzi wote, ili ikapandwe katika mlima wenye mawe pale Ilula. Wazo hili ni zuri, ila kuna wakati huwa halifanikiwi. Suala la kugawa miche ya miti na kuwalazimisha watu kuipanda sio mara zote linafanikiwa. Suala hili linategemea sana mazingira ya eneo husika, mwamko wa watu wa eneo hilo na uhusiano wa mamlaka inayogawa miche na wananchi wa eneo husika. Mfano, kati ya mwaka 1981 – 2000, mradi wa ‘Soil Erosion Control and Agroforestry Project’ (SECAP) ulianzishwa na kuendeshwa katika milima ya Usambara, hususan wilayani Lushoto. Mradi huu ulikuwa la lengo la kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na nyasi katika maeneo mbali mbali ya milima hii ya Usambara. Katika baadhi ya vijiji wanavijiji walipewa miche ya miti na mbegu za majani ya kulisha mifugo, baadhi yao walitupa miche na mbegu hizo na kufanya mradi kutokuwa endelevu. Vijiji ambavyo nilivipitia mwezi Juni mwaka 2005 na walikiri kufanya hivi, (pengine kwa kutojua faida za mti kwa wakati huo) ni Boheloi, Yamba, Mazashai (kata ya Gare) na vijiji vya Mambo, Makose na Mamboleo (kata ya Mtae). Vipara vilivyo katika maeneo haya vinasikitisha sana, hasa ukizingatia kuwa kulikuwa na mradi mkubwa wa utunzaji wa mazingira kwa miaka takribani ishirini. Huu sio uzushi, ila ni hali halisi, kama kuna mtu anatoka maeneo tajwa ama amepita maeneo hayo na kuongea na wenyeji, anaelewa nini ninaongelea hapa. Kuna miradi kadhaa inayofanana na huo wa SECAP ilifanyika katika wilaya ya Mbeya, ambayo ilifadhiliwa na iliyokuwa 'European Economic Community-EEC sasa inaitwa 'European Commission'-EC, ilifanikiwa. Nitatoa makala ya miradi hii siku za baadae kidogo.

2. PENDEKEZO LA KUWA NA SIKU MAALUM YA KUPANDA MITI
Kuna wanakiji walipendekeza kuteuliwa kwa siku maalum ya kupanda miti. Tayari siku hii tunayo, kwani kila ufikapo tarehe mosi mwezi Januari kila mwaka kunakuwa na kampeni za kitaifa za kupanda miti. Ni miti mingi inapandwa katika siku hii na watu binafsi, mashirika, serikali na taasisi mbali mbali. Baada ya kupanda miti suala la ufuatiliaji kujua hali ya mimea hii huwa duni sana, kiasi kwamba mingi ya miti hii huwa inakauka kwa kukosa matunzo. Suala la kupanda miti halina ubaya wowote na ni wazo zuri sana. Lakini sasa, baada ya kupanda, ni nani anajipa shida ya kujua hali ya miti hii baada ya kampeni hizi? Mara nyingi tunapanda miti katika kampeni wakati wa mvua za masika, lakini ni nani anajipa shida ya kufuatilia miti hii mara baada ya mvua za masika kwisha? Nani anakuwa na uhakika kuwa mizizi ya miti hii inakuwa imeshika vyema na ina uwezo wa kufyonza maji sasawasawa wakati wa kiangazi? Ni miji michache sana ambayo hufanya ufuatiliaji wa miti hii mara baada ya kampeni hizi. Kiujumla inatakiwa kila mwananchi awe na mwamko wa kutunza mazingira ya eneo husika, badala ya kusubiri kampeni, ambazo aghalabu huwa ni za zimamoto ama za muda mfupi.

3. MJADALA WA UMILIKI WA ENEO HUSIKA
Niwe wazi kuwa sina uhakika kuwa ni nani anamiliki eneo la Ilula lililoachwa wazi bila mimea. Huenda ikawa ni eneo lililo chni ya mamlaka ya halmashauri ya manispaa, halmashauri ya kijiji ama serikali kuu. Tangu miaka ya nyuma hasa baada ya Azimio la Arusha la mwaka 1967, sehemu kubwa ya ardhi ya nchi yetu ipo/ilikuwa katika miliki ya serikali kuu. Hii inajumuisha pamoja na mambo mengine vitu vyote vilivyomo katika ardhi hiyo, kama vile maji, madini, mimea na wanyama. Ni hivi majuzi tu ambapo maeneo haya yameanza kumilikishwa kwa serikali za mitaa, zikiwemo serikali za vijiji. Suala hili la ardhi kuwa chini ya serikali kuu lilifanya watu kuvamia maeneo haya na kufanya wanachokitaka ikiwa ni pamoja na kuchukua rasilimali zilizomo kama vile kuchimba madini, kurina asali, kuwinda, kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, kupasua mbao na mara nyingine kuichoma moto. Ilikuwa ni ‘Tragedy of the Commons’, kwamba mali ya umma haina hasara. Mara nyingi madhara ya vitendo hivi yametupata hata tusiohusika, kwa hiyo ndio sababu inayotufanya tunapiga kelele. Suala la kuacha kila kitu chini ya serikali kuu siliafiki sana. Tunasema kuwa “Serikali ina mkono Mrefu”, sawa lakini mkono huu una kikomo na kuna maeneo ambayo huwa mkono huu wa serikali kuu hauwezi kufika. Waliowahi kufanya kazi vijijini ambako hata baiskeli hakuna wanaelewa ninachoongelea hapa. Kuna baadhi ya vijiji Tanzania havifikiki kwa magari wala baiskeli, kwa hiyo kusema serikali kuu itafika maeneo hayo na kutekeleza yale wananchi wanayotaka sio kweli. Lazima mambo mengine yaliyo ndani ya uwezo wa serikali za vijiji yaachwe chini ya mamlaka ya serikali za vijiji. Kwa hiyo basi, maeneo kama haya yakipewa umiliki binafsi wa serikali za vijiji yatatunzwa na kuheshimiwa, kwani huku vijijini ndiko serikali inakoanzia na ni wanavijiji ambao ndio waathirika wa kwanza wa moja kwa moja wa athari chanya na hasi za vitendo nilivyoongelea hapo juu, na wengine tunafuata. Kuna wanakijiji wameponda sana suala hili, lakini kamwe hii hainizuii mimi kuendelea kusimamia hoja hii kwa miguu yote. Hatuwezi tu kukurupuka leo na kwenda kupanda miti katika eneo husika eti kwa sababu mvua za masika zinanyesha, bila kujua mmiliki wa eneo husika na bila kujua ana mpango gani na eneo hilo. Huku ni kukurupuka. Naunga mkono suala la kupanda miti, lakini lazima tujue tunapanda miti katika eneo la nani, isije kuwa tunatafuta kesi kwa kuvamia eneo la mtu.

4. MBINU SHIRIKISHI
Pamoja na kwamba kumekuwa na mawazo mbadala kutoka kwa wanakijiji kuhusu hoja hii, lakini pia ina umuhimu wake kwa mazingira ya sasa. Watanzania wa leo huwa wanahoji kila suala, hata kama hawachukui hatua katika suala hilo, lazima wajue nini kinaendelea. Siafiki suala la kuwapita kando ‘by-pass’ wakaazi wa eneo husika. Watanzania wa leo ukiwalazimisha suala ambalo hawalitaki huwa wanasema hapo hapo! Wamebadilika! Kwa hiyo basi, iwapo tunataka kupanda miti eneo la Ilula lililothiriwa, lazima tuwashirikishe wananchi. Narudia kusema kuwa, waliokata miti kwa ajili ya kuni, mbao, ujenzi, uchomaji wa mkaa na kadhalika huenda hawakutoka mbali na hapo, kwa hiyo ni hao hao. Kwa hiyo basi, naunga mkono hoja ya wao kushirikishwa katika kuhuisha mimea ya eneo husika. Nilitoa mfano wa mradi wa “Communal Areas Management Programme For Indigenous Resources” (CAMPFIRE) ulio nchini Zimbabwe, kuwa walitumia mbini hii katika kutekeleza mradi huo na walifanikiwa, kwa nini na sisi tusitumie mbinu hii kama inawezekana? Soma zaidi hapa http://www.resourceafrica.org/documents/1993/1993_campfire_bg.pdf kuhusu mradi huu.
Mfano mwingine wa mbinu shirikishi katika utunzaji wa mazingira unaweza kuusoma hapa, 'http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/9/13/habari33.php' Kitendo cha kufanya mambo ambayo yatawaathiri wananchi hapo baadaye bila kuwashirikisha ni dharau na kinaweza kuleta madhara. Hali kadhalika kitendo hiki kinawaweka wananchi nje ya mradi husika, hivyo wanakuwa hawana uchungu na mradi huo. Ndio hapa vurugu inapoanza, ni katika hatua hii uwindaji haramu hutokea, uchomaji wa mkaa kinyemela hufanyika, ukataji miti bila vibali hutokea na vitendo vingine vinavyofanana na hivyo. Ushirikishwaji wa jamii “Local Level Planning” haukwepeki kwa suala kama la Ilula, kwa hiyo hatuna budi kulipa nafasi yake katika mchakato huu mzima wa kuhuisha eneo husika. Tukidhani kuwa wao hajui mbinu bora za kuhuisha eneo hili tutakuwa tunawakosea haki. Sio vibaya kama tutakumbuka malalamiko ya wananchi wakati wa ‘Operesheni Vijiji/sogeza’ ya miaka ya sabini. Je miradi yote iliyoanzishwa na serikali katika operesheni hii bado inafanya kazi?

5. UREJESHWAJI WA MIMEA ASILIA
Kwa sababu wataalamu wa kwanza na wa kuaminika kwa mtazamo wangu ni wanakijiji wa eneo husika, naamini wao ndio wanaojua ni miti ama mimea ya namna gani ilikuwa inastawi katika eneo husika. Kwa hiyo basi, iwapo wazo ni kurejesha mimea katika eneo husika, sio vibaya kama ile mimea ya mwanzo (original indigeneous species) ikapewa kipaumbele,ndipo mimea mingine hamiaji (exotic species)ipewe nafasi. Inawezekana mimea ya mwanzo isikubali katika eneo husika kulingana na ukubwa wa athari, lakini pia mimea vamizi ina athari zake, na huenda isistawi vyema. Inabidi tuwe makini na hili, kwani tusije kurudi kule kule, leo tunapanda miti na baadaye kidogo tunaambiwa tukate kwa sababu inahatarisha vyanzo vya maji. Hii yote inatokana na kukurupuka. Nadhani tunakumbuka vyema habari ya mikaratusi, kwamba ilipandwa kwa lengo jema kabisa lakini ‘wataalamu’ sijui wa namna gani wakasema miti hii inaharibu vyanzo vya maji. Hoja hii niliipinga wakati fulani bloguni hapa. Nisingependa sana turejee huku miaka kadhaa ijayo.

HITIMISHO
Hatima ya michango ya wanakijiji iwe ni kuhakikisha kuwa eneo tajwa linabadilika kutoka hali ya jangwa iliyopo sasa na kuwa mahali penye mimea. Lakini tisifanye suala hili kwa kukurupuka, kama ilivyo jadi ya Watanzania wengi, tutafeli. Narudia kusema kuwa kijiji (blogu) na wanakijiji kwa ujumla tuna lengo la kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili. Lakini utatuzi huu lazima uwe ‘credible’, vinginevyo tutakuwa tunatwanga maji katika kinu.
Nawasilisha.

MABADILIKO YA HALI YA TABIANCHI

UTANGULIZIMnamo tarehe 18 Septemba 2007, nilihudhuria semina kuhusu mabadiliko hasi ya tabianchi na madhara yake katika viumbehai na katika maisha ya mwanadamu kwa upekee. Semina hii ilifanyika katika jiji la Oslo, Norway na ilishirikisha wadau wa taaluma mbali mbali kama vile wanasosholojia, wahandisi, wasanifu, wanasiasa, wataalamu wa ardhi na maji na wataalamu wa mazingira, kwa kutaja wachache, kutoka mabara yote. Hakika ilikuwa ni semina nzuri sana, kwani kulikuwa na mijadala mikali sana hasa kuhusu namna ya kuyakabili masuala haya kwa undani na kwa mbinu zinazokubalika katika mazingira ya sasa. Tulipata wasaa wa kuangalia picha za video zilizopigwa nchini Kenya, Nepal, Norway na Uganda, na wahusika toka nchi hizi ndio walikuwa wazungumzaji wakuu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, kadri walivyoshuhudia toka katika nchi zao.


MADAMtoa mada Joseph Kones kutoka Kenya aliwasilisha ushuhuda wake wa mabadiliko ya hali ya hewa kutoka mahali alipozaliwa, eneo la Maasai Mara, lililo katika bonde la mto Mara. Ikumbukwe kuwa bonde hili limesambaa mpaka Tanzania, katika mbuga ya wanyama ya Serengeti. Akasema kwamba kati ya miaka ya hamsini na sabini kulikuwa na mvua za kutosha na zilikuja kwa msimu maalum. Kwamba, mvua za masika zilikuwa inanyesha kuanzia mwezi Machi hadi Mei na ndio msimu ambao wakulima walipanda mazao yao. Lakini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa ya hivi karibuni, hali imekuwa sio hiyo tena, kwani kwa sasa mvua za masika hazina msimu maalum kwa eneo hilo, ambalo kwa sasa linakabiliwa na ukame wa mara kwa mara. Pia mvua zinazonyesha katika eneo hilo kwa sasa hazina kiwango maalum kama zamani, kwamba zinaweza kuja nyingi na kusababisha mafuriko, ama zikaja chache na kutotosheleza mahitaji ya mimea, ama zisije kabisa katika msimu husika kiasi cha kusababisha ukame. Hali kadhalika, mtoa mada aliongelea suala la mbu waletao malaria, kwamba katika kipindi tajwa hapo juu kulikuwa hakuna mbu wa malaria katika eneo hilo, lakini kuanzia mwishoni mwa miaka ya themanini kumekuwa na malaria katika eneo hilo. Kutokana na ukame wa mara kwa mara, kumekuwa na baa la njaa ambalo husbabishwa na mazao kukauka kabla ya kukomaa, mifugo inakufa kutokana na kukosa malisho na kukauka kwa vyanzo vya maji kwa ujumla. Hali kadhalika, kumekuwa na ugomvi wa mara kwa mara kati ya jamii za wafugaji wa Kipsigi na Wamasai, kugombea malisho na maeneo ya kunyweshea mifugo yao. Kumekuwa pia na magonjwa yanayosambaa kwa njia ya maji, kama vile kichocho na homa za matumbo. Kumekuwa na uchafuzi wa mito na vyanzo vya maji, kutokana na wingi wa mifugo usioendana na uwezo wa vyanzo hivi kukidhi idadi hii ya mifugo. Akatoa wito kwa jumuiya za kimataifa pamoja na wadau wengine, kuangalia namna ya kuyaokoa maeneo haya kutokana na athari hizi.

Naye mtoa mada Frank Turyatunga (mwakilishi wa UNEP) kutoka nchini Uganda alikuwa na yake ya kusimulia kutoka nchini mwake. Alisema kwamba kuna mto unaotenganisha nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda. Mto huu enzi za miaka ya sitini na sabini ulikuwa hauathiriwi sana na mafuriko ya mara kwa mara, lakini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa sasa mto huo hufurika mara kwa mara na unamomonyoa kingo zake na kusababisha eneo kubwa la ardhi ya kumegwa na kusombwa na maji, na wakati mwingine mto huhama na kumega eneo la Uganda. Hali hii inasababisha Uganda kupoteza ardhi yake, kwani mto huu ni mpaka kati ya nchi hizi mbili, kwa maana hiyo kama mto unahama na kuelekea upande mwingine basi nchi nyingine hufaidi sehemu ya ardhi ambayo imehamwa na mto. Ikumbukwe kuwa eneo hili pa limegunduliwa kuwa na utajiri wa mafuta, kwa hiyo inaweza kuwa chanzo cha migogoro hapo baadaye. (Zingatia kuwa mto Songwe ulio kati ya nchi za Malawi na Tanzania una tabia ya namna hii, ya kuhama mkondo mara kwa mara kiasi cha kusababisha matatizo katika eno husika)

Mtoa mada Norbu Sherpa kutoka Nepal alikuwa na yake ya kuzungumza, hasa kutokana na athari za mafuriko ya mara kwa mara kutokana myeyuko wa barafu kutoka katika kilele cha milima ya Himalaya, unaochangiwa na ongezeko la joto duniani. Huyu alitoa ulinganifu wa athari kwa kufuata miaka, kama nilivyotaja hapo juu. Kwa ujumla mtoa mada huyu alilalamikia suala la kumegwa kwa ardhi kando ya kingo za mito, kiasi cha kuwalazimu wao kuhama maeneo hayo na kuelekea maeneo ambayo yana mwinuko zaidi, ili kujiepusha na athari za mafuriko hapo baadaye. Aliongelea suala la kusombwa kwa mazao, makazi na kupotea kwa maisha ya watu kutokana na mafuriko.

MJADALAShuhuda zilizojadiliwa hapo juu ndio zimekuwa kilio cha nchi nyingi duniani na athari hizi hata nchini mwetu zinaonekana waziwazi. Vimbunga vya mara kwa mara (1995), mafuriko (kumbuka el nino 1997/1998), ongezeko la magonjwa, ukame wa mara kwa mara (1993/1994) , (2005/2006) na ongezeko la joto ni baadhi tu ya athari za mabadiliko tajwa ya hali hewa. Ukiachilia ushuhuda wa uzoefu kutoka kwa wazee wetu na wakaazi wa maeneo mbali mbali, kuna mbinu za kisayansi za kupima mabadiliko haya hasi ya hali ya hewa na athari zake. Mbinu hizi zipo nyingi sana, ila nitagusia chache tu kwa ufupi. Mbinu hizi ni kama zifuatazo.

Ongezeko la JotoOngezeko la joto (mean annual temperature) hupimwa kwa kutumia vipimajoto vya satelaiti pamoja na vile vilivyo ardhini katika vituo vya hali ya hewa na kufanyiwa ulinganifu wa kitaalamu (modelling) kutoka wakati mmoja na mwingine ama kutoka mwaka mmoja na mwingine. Mfano, vipimo vya vilivyochukuliwa miaka ya arobaini hadi miaka ya sitini hulinganishwa na vile vinavyochukuliwa sasa na kukokotoa tofauti yake. Mara nyingi athari za ongezeko hili la joto ni pamoja na kuongezeka kwa myeyuko wa barafu ambapo husababisha mafuriko, kusambaa kwa magonjwa kama vile malaria na kukauka kwa vyanzo vya maji. Si ajabu basi tukisikia kuwa maeneo kama Kitulo, Makete, Mufindi ama Marangu hayakuwa na mbu waletao malaria katika miaka ya sitini na sabini lakini sasa kuna malaria!

Kupungua kwa kasi ama Kupotea kwa jamii za MimeaKuna baadhi ya mimea ambayo huwa inaathirika sana kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Upotevu huu hupimwa kulingana na wakati na kufanyiwa ulinganifu. Kwamba kwa mfano, kama mwaka 1930 kulikuwa na mimea 20 ya aina fulani katika meta moja ya eneo, na kwa sasa kuna mimea 8 ya jamii hiyo katika eneo hilo hilo la meta moja ya eneo, basi tunaweza kujua kwamba upotevu wa mimea ni kiasi gani kwa kufanya ulinganifu sasa, tangu eneo hilo lilipowekwa kumbukumbu ya mimea hiyo. Kwa sababu mimea na wanyama hushirikiana katika ikolojia na mfumo lishe, athari kwa mimea pia huleta athari kwa wanyama. Iwapo mimea mingi inakuwa imeondolewa katika eneo fulani , maji hayawezi kutunzwa ardhini, kwani mimea husaidia kutunza maji kwa kuzuia mionzi ya jua kutua moja kwa moja ardhini. Zingatia kwamba eneo tajwa linalofayiwa utafiti niliotaja hapo juu ni lile ambalo halijaathiriwa na shughuli za moja kwa moja za binadamu kama kilimo, ukataji miti na upandikizaji wa mimea mipya.

Mtawanyiko wa MajiKila eneo la ardhi duniani lina mtawanyiko wake maalum wa maji (surface run-off) kwa kila kilometa ya eneo. Kadri athari za kimazingira zinavyoongezeka ndio mtawanyiko huu hupungua ama kuongezeka. Kwa ufafanuzi ni kwamba, joto likichanganyikana na upepo huongeza kasi ya upumuaji (evaporation) ya mito na maziwa, hivyo kupunguza uwingi wa maji. Iwapo ongezeko hili ni la kudumu, basi na upungufu huu huwa ni wa muda mrefu. Hali kadhalika kwa maeneo yenye barafu, iwapo kutakuwa na ongezeko la joto, basi myeyuko wa barafu huwa ni wa kiwango cha juu na huenda ukawa ni wa kudumu hivyo kuongeza uwingi wa maji wa eneo husika, hasa wakati wa joto. Vipimo vya maji vya eneo husika ndivyo hufanyiwa ulinganifu kutokana na wakati na kutathmini athari zake.

Kutokana na athari hizi basi, kumekuwa na mwamko katika maeneo mbali mbali hapa duniani kuhusu namna bora ya kukabili athari za uharibifu wa mazingira na ongezeko la joto.
Tufanye nini basi ili kukabiliana na athari hizi? Nini kifanyike ili vyanzo vya maji visikauke? Tufanye nini ili mvua zije kwa wakati na za kutosha? Jadili.

JUMUWATA

Ndugu msomaji wa blogu hii, Jumuiya ya Wanablogu Tanzania (JUMUWATA) inakaribisha mchango wa mawazo yako wa namna ya kuiboresha.
Mchango wako unahitajika sana wewe mwenye blogu na hata usiye na blogu ilikujenga muelekeo uliochangiwa na wengi na sio kikundi cha watu wachache.Karibu uchangie, kosoa,kemea,shauri, ondoa, .... ilikupata muelekeo na jumuiya ya wanablogu Tanzania unayoweza kujivunia.Kama unablogu tunaomba uweke tangazo la kuwafahamisha watu kuhusu ombi la mchango wao wa mawazo hapa ili liwezekuwafikia watu wengi.
KARIBUNI WOTE!
Imetolewa na,
Uongozi wa JUMUWATA

KADHIA YA ONGEZEKO LA JOTO

Utangulizi
Kumekuwa na matukio mbali mbali yanayotokea mahali mbali mbali duniani kama kiashirio cha mabadiliko ya hali ya hewa katika uso wa dunia, ikiwemo vimbunga, mafuriko, ukame, kuongezeka kwa kina cha maji baharini, upotevu wa jamii za mimea na wanyama na kuyeyuka kwa barafu katika mzingo wa Aktiki ulio kaskazini mwa dunia. Haya ni baadhi tu ya matukio ambayo ni viashiria, kwamba inatupasa kucukua hatua za makusudi kukabili hali hii.

MADA
Kwa huku upande wa kaskazini mwa dunia, kumekuwa na malalamiko ya ukosefu wa theluji katika msimu mwafaka. Kwa kawaida, kwa tropiki ya Kansa msimu wa baridi huanza mwezi Novemba. Wenyeji wa huku huwa wanapenda sana kuteleza katika theluji na imezoeleka kila mara kwamba kila ifikapo mwezi Desemba basi kila mahali huwa na theluji ya kutosha kwa sababu joto huwa chini ya nyuzi sifuri, na kila mtu hufurahia hali hii. Lakini kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko yasiyo ya kawaida katika hali hii, kwamba kwa sasa inatokea kwamba ifikapo Desemba kunakuwa hakuna theluji kabisa na joto linakwa liko juu ya nyuzi sifuri. Kwa maana hiyo, msimu wa baridi umekuwa mfupi sana ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Wenyeji wanasema kuwa mabadiliko haya hasi yameanza hasa kuonekana kuanzia mwaka 1986 na kuendelea, na hali inazidi kuwa mbaya kadri miaka inavyozidi.
Kwa upande wa tropiki ya Kaprikoni, chini ya Ikweta, huku ndio huwa na ukame uliokithiri, kutokana na mabadiliko haya. Ikumbukwe kwamba mnamo mwaka 2005 kulikuwa na ukame ambao uliathiri sana upatikanaji wa maji, kiasi cha kusababisha matatizo katika uzalishaji wa umeme. Kwa mujibu wa baadhi ya tafiti za kitaalamu, hali hii huenda ikawa ni matukio ya kawaida iwapo nchi zinazoongoza kwa uchafuzi wa hali ya hewa hazitafanya juhudi za makusudi katika kupunguza hewa ya kaboni dayoksaidi itokayo katika viwanda vyao.
Inapaswa kila mtu ajivike majukumu ya kukabiliana na hali hii kwa kufanya yafuatayo.

1. Utunzaji wa Nishati
Kuzima vifaa vya umeme kama vile taa, pasi, runinga, majiko na feni ama viyoyozi iwapo kwa muda huo vinakuwa havihitajiki. Hii husaidia kupunguza matumizi ya nishati yasiyo ya lazima, hivyo kupunguza pia uzalishaji wa nishati husika.

2. Kutumia Usafiri wa Jumuiya
Iwapo kunakuwa hakuna ulazima wa kutumia usafiri binafsi, basi ni vyema kama tutatumia usafiri wa jumuiya kama vile mabasi, treni na meli kwa safari zetu mbali mbali. Kitendo hiki kitapunguza kiwango cha nishati kitumikacho na mitambo hii. Kitendo hiki kiende sambamba na matumizi ya baiskeli kwa safari fupi fupi ambazo hazimlazimu mtu kutumia gari ama pikipiki.

3. Utunzaji wa Maji
Tutumie maji tuliyonayo kwa kujibana. Hii itasaidia sana kupunguza matumizi yake, kiasi kwamba yale machache tuliyo nayo yanaweza kabisa kututosha. Pia ni vyema kama tutakuwa na utaratibu wa kusafisha maji yaliyokwisha kutumika, ili yatumike tena kwa matumizi mengine kama vile umwagiliaji wa mashamba na ujenzi.

Inawezekana, tutimize wajibu wetu.